NGUVU YA ULICHONACHO
THE POWER OF YOUR POSSESION!
NGUVU YA ULICHONACHO!
|
1
|
YALIYOMO;
SEHEMU YA KWANZA……….MATOKEO
YANAYOSABABISHWA NA ULICHONACHO.
SEHEMU YA PILI……………………...UMILIKI WA FANI NA UJUZI
SEHEMU YA TATU……………………..WEWE NI NANI?
SEHEMU YA NNE……………………..UNA NINI MKONONI MWAKO?[MTAJI]
SEHEMU YA TANO……………………NAMNA YA KUANZA KUTUMIA ULICHONACHO
SEHEMU YA SITA ……………………..SHUKRANI
SEHEMU YA SABA…….………………..KUHUSU MWANDISHI,
SEHEMU YA KWANZA
MATOKEO YANAYOSABABISHWA NA
ULICHONACHO.
Kila kitu ambacho unakimiliki
huwa kina uwezo wa kukuletea matokeo ya aina kuu mbili
Yaani matokeo haya ni
·
Kukuinua[kukupandisha viwango vya mafanikio
yako]
·
Kukuharibu .[kukushusha chini]
Haya ni matokeo ambayo huwezi
kuyakwepa maana kwa vyovyote vile ni lazima mojawapo likupate
Mfano 1
Ukimiliki gari linaweza kukufanya
aidha ukawa masikini kwa sababu ya gharama ya uendeshaji au ukawa tajiri kwa
sababu ya matumizi sahihi ya hilo gari lako
Hasa kama utalitumia gari lako
kuzurula mtaani na kumaliza mafuta bila kuwa na chanzo kizuri cha kukuingizia
kipato.
Mfano 2.
Ukiwa na mume au mke anao uwezo
wa kukufanya aidha uone dunia ni mahali sahihi pa kuishi kwa amani kama mbingu
ndogo
au
Anao uwezo wa kukufanya uone
dunia ni jehanamu ndogo unapoisubiri iliyokubwa.
Kwa mifano hii unaweza kuona kwa
kila unachokimiliki huwa kuna nguvu ya ndani ya aidha kukuletea matokeo chanya
au hasi katika maisha yako.
Mfano 3
Unaweza ukapata watoto katika
ndoa yako lakini watoto wako wakafanyika kuwa mwiba katika maisha yako hadi
ukafikia wakati wa kujuta ni kwanini Mungu amekupatia watoto.
Lakini pia ufahamu kuwa unaweza
kupata watoto halafu watoto wako wakakufanya uone furaha ya kuwa na watoto wako.sasa kila kitu huwa kina
nguvu aidha ya kukufanya ufurahi au ulie.
Kati ya watu ambao ninadhani
walipata shida sana na pengine walijilaumu sana kwa matokeo yaliyosababishwa na
wanavyo vimiliki ninadhani mojawapo ni ADAMU
Mwanzo 3;1-7
Katika kitabu hiki cha mwanzo
sura ya 3, Biblia inaeleza kwa habari ya majanga makubwa ambayo mke wa Adamu
aliweza kumsababishia mumewe na akajisababishia nayeye mwenyewe pia.
Ni baada ya kudanganywa na Yule
nyoka[shetani] na hatimaye akavunja sheria za Bustani ya Edeni,mwishoni
wanafukuzwa kukaa Edeni na kupewa adhabu ya kula kwa jasho na kuzaa kwa
uchungu.
Mfano mwingine ni ule wa Samsoni na Delila
Tunaona jinsi ambavyo yawezekana
samsoni alijuta sana kuwa na Delila kama mke wake baada ya kuingia katika mateso
makubwa kwa sababu ya Yule Delila.
Sasa hiyo ni baadhi tu ya
mifano,lakini unaweza kuoa mwanamke au
kuolewa na mwanaume anayeweza akabadilisha kabisa historia ya maisha yako kwa sababu ya tabia
mbalimbali ambazo mtu Yule anazo ,hatimaye ukaingia katika matatizo.
Kupitia kitabu hiki,tunajifunza
vile Samsoni alivoweza kufanyiwa kitu kibaya na cha kinyama kabisa na mwanamke
aliyempenda sana[ Delila],unaweza ukafikiri ni kwa jinsi gani inavyoumiza
kusalitiwa na mtu unaye mpenda sana.
Naweka mkazo kukutaarifu kuwa ,watu ulionao au kitu
ulichonacho kina uwezo wa kubadilisha hatima ya maisha yako katika namna chanya
au namna hasi.
2.SHERIA ZA UMILIKI HALALI
Ili uweze kumiliki kitu kiuhalali
kuna vigezo au sheria ambazo nilazima uzipitie,pasipo kupitia hizi hatua
utapata shida sana kwa sababu ule
umiliki wako utakuwa unakosa baadhi ya vionjo.Ingekuwa ni chakula tungesema ili
chakula kiwe kitamu kuna vitu vinatakiwa viwepo kama vile chumvi,mafuta
,vitunguu n.k.
A. NI LAZIMA UINGIE GHARAMA YA UNACHOKIMILIKI
Kuna watu huwa wanapenda kumiliki
vitu viwe vya kwao ,lakini kwa bahati mbaya hawataki kupitia ule mchakato wa
kuingia Gharama ya umiliki halali.Mfano mzuri , unaweza kununua kiwanja ,lakini
ukaona uvivu kwenda kwa watu wa ardhi ili wakupimie na kukupatia hati miliki
inayokutambulisha wewe kuwa mmiliki halali wa kile kiwanja.
Sasa ili ufanikiwe kuwa mmiliki
halali ni lazima uwe na hati ya kwako, malizia kulipa gharama zote za lazima
ili uwe na kitu cha kwako mwenyewe.Jambo hili wala sio la kibinadamu au kimwili
sana,hata biblia inasisitiza maeneo mengi sana, na inatoa mifano ya watu ambao
walilazimika kuingia katika gharama za lazima katika umiliki wao.Kwahiyo usiwe
mjinga ,unavoenda katika umiliki wa mambo hakikisha una kamilisha kulipa gharama zote za umiliki halali.
KUTOKA KATIKA BIBLIA
Yeremia 32;9
Huyu jamaa alinunua shamba
,akalipa gharama ya lile shamba akapewa na hati yake. Sasa wewe ni nani hata usione umuhimu wa
kulipa gharama ya unavyovimiliki na hatimaye ukapewa hati za kwako za umiliki
halali?.
Mwanzo 23;16-18
Hapa utakutana na Ibrahimu baba
wa Imani ,ambaye na yeye hakuwa nyuma , aliamua kulinunua shamba katika makpela
,na akaandikishana na mashahidi na akapewa hati yake halali ya umiliki halali.
Hatuna sababu ya kujitetea wakristo
kwa kushindwa kumiliki vitu vyetu kiuhalali.pambana hadi upate umiliki halali
,kubali kulipa gharama ya vile unavyotakiwa kuvimiliki.
B. TAFUTA MASHAHIDI HALALI WAKATI WA KUMILIKI
Mashahidi ni watu muhimu sana
ambao wanakuwa na uwezo wa kukutetea wewe wakati ambao unakutwa na changamoto za
vile unavyo vimiliki.
Hata katika kesi nyingi za
migogoro ya Ardhi,kuna mambo mengi huwa yanatokea ,unaweza kuzulumiwa mali
ambayo ni halali yako ,lakini kwa sababu hauna mashahidi wa kuthibitisha kuwa
ulichinacho ni cha kwako.
Hata ndoa, huwa zinakuwa na
mashahidi halali,na ndiyo maana hakuna ndoa halali ambayo huwa inafungwa
pasipokuwa na mashahidi.
Mungu anatambua umuhimu wa
mashahidi katika kila kitu tunachokifanya ,na ndiyo maana tunatakiwa kufuata
utaratibu huu wa kutafuta mashahidi halali katika kila kitu tunachokimiliki.
KUTOKA KATIKA BIBLIA
Hili jambo ni la kiroho kabisa
,na Mungu hapendi wakristo wajinga wajinga wasiofahamu kanuni na taratibu
zinazotakiwa kufuatwa katika umiliki halali.
Yeremeia 32;9-10
Mwanzo 23;17-19
Bado katika mifano hii utaona
jinsi ambavyo mashahidi wanatakiwa katika kila kitu au thamani uliyo nayo.Mungu
atusaidie sana wakristo tuweze kuwa makini katika vitu ambavyo Mungu wetu
ametupatia tuvimiliki.Tafuta mashahidi halali!.
C. KUBALI MAUMIVU MAANA YANAKUJENGEA UMILIKI
WA NDANI
Ili uweze kuwa mmiliki halali
,gharama ya maumivu ya kile kitu unachobeba pia inahusika sana kukutengenezea
saikolojia ya kukimiliki na kukitunza kile kitu.
Mfano
Kuku huwa ana atamia mayai yake
kwa muda wa siku 21.Katika siku hizo 21,kuku huwa anakubali kushinda njaa na kukaa eneo moja kwa muda mrefu
sana,hata kama kuna hatari, kuku huwa anakaa akiwa amelalia mayai yake
hivyohivyo.
Baada ya siku 21 kuku hutotoa
vifaranga wake,sasa kuanzia hapo wewe jifanye unajipitisha karibu ya Yule
kifaranga wa kuku ,utadonolewa ndugu yangu hata kama ni mtu mzima lazima
utakuwa na ile hofu Fulani maana ule umiliki unampatia nguvu na utisho dhidi ya
maadui zake.
Sasa ile gharama ya maumivu
uliyoipata wakati wa kujiandaa kumiliki ulichonacho huwa inachangia sana wewe
kukupatia umiliki halali na umakini wa
vitu unavyo vimiliki,inakuongezea ule umakini wa ndani.
KUTOKA KATIKA BIBLIA
Mathayo 1;25
Mariamu anakuwa mama wa Yesu
[cheo kikubwa sana hicho] kwa sababu ya ile gharama ya kubeba ujauzito wa Bwana
Yesu kwa muda wa miezi tisa hadi akajifungua mtoto wa kiume.
Anasimama kifua mbele pamoja na
Yusufu Kumtetea Bwana Yesu dhidi ya Yule
Herode aliyetaka kumuangamiza ,Mariamua na Yusufu wanakimbilia Misri kumtetea
Yesu ambaye ni mtoto wao kwa sababu kuna
gharama alilipa kumpata Yesu ,na ndiyo inampatia uhalali wa kuwa mama wa Yesu.
Kuna mwanamke gani ambaye anazaa
kwa uchungu halafu hamtetei mtoto wake anapopita katika changamoto ?
Najua wapo wazazi ambao hata hawajali watoto wao ,lakini ukweli
ni kwamba wanatakiwa kuwalinda na kuwatetea watoto wao.
SEHEMU YA PILI
UMILIKI
WA FANI NA UJUZI
Fani
au ujuzi Fulani ni kile kitu ambacho mtu ameumbiwa kukifanya hata kabla
hajaenda shule
Ningeweza
kusema ni uwezo au ujuzi asilia wa kufanya kitu Fulani .watu wengine huenda
mbali wakasema ni kile kipaji maalumu ambacho mtu anazaliwa nacho.
Maana
ya kuzaliwa nacho ni ya kibinadamu,lakini Kimungu tunasema ni kupewa na Mungu.
Sasa
kile kitu ambacho usipokifanya unasikia kama kuna kitu kinakosekana moyoni
mwako[kile unachokipenda kuliko vitu
vyote] kinaitwa kipaji au fani yako
Mifano
ya baadhi ya fani za watu
·
Fundi cherehani hodari
·
Mchezaji wa mpira hodari
·
Mpigaji wa kinanda hodari
·
Mpika maandazi hodari
·
Mwimbaji hodari
·
Mkulima hodari
·
Mchungaji hodari
·
Mwana riadha hodari
Na
vingine vingi sana.hiyo hodari niliyoiweka mwishoni mwa kila kipaji wala
isikusumbue,nimeitumia tu ili iweze kukupatia hamasa,maana natambua kabisa kuwa
kila kitu huwa kinaanzia chini kisha kinapanda juu,wala usiwe na hofu hata kama
wewe bado hujafika katika ngazi ya uhodari ,waweza kuanzia hapohapo chini halafu
ukajikuta mwisho wa siku umepandishwa viwango kabisa.
Sasa
kitu cha muhimu hapa ni kujua fani yako au kipaji chako wewe ni kipi?
Ushuhuda!
Kuna rafiki yangu mmoja ,baba
yake alijitahidi sana kumpeleka shule ili akasome.Na alimpeleka shule ya
sheria,
Cha kushangaza sana Yule
jamaa alikuwa anenda shule asubuhi ,ikifika mchana kabla yavipindi kuisha
anatoroka na kurudi nyumbani,kwenda
kushughulikia mifugo yake ,maana alikuwa ameanza mradi wa kufuga nguruwe.
Waligombana sana na baba yake
,kwa maana kila aliporudi nyumbani , baba yake alimsema na kumkaripia sana
,Yule kijana kwa kumuonea huruma baba yake ,aliamua kuendelea kusoma kwa bidii
ili tu amalize chuo salama.
Ni kweli kama ilivyo kawaida
,lisilo na mwanzo halikosi mwisho,Yule kijana alihitimu shule sal,na akapata
ufaulu wa kawaida tu.
Sasa baada ya kuhitimu chuo
,akiwa na shahada yake ya kwanza ya sheria ,mchakato wa kutafuta kazi
ukaanza,alizunguka kwenye taasisi nyingi
na kwenye maofisi ya watu mbalimbali lakini hakupata kazi.
Alimlaumu sana babayake kuwa
kwanini alimlazimisha kusoma fani asiyoitaka na tena fani yenyewe haina hata
ajira?
Baadaye alikata tamaa akaamua
kurudi kwenye mradi wake wa kufuga nguruwe.
Cha kushangaza ndani ya muda
mfupi sana ,rafiki yangu alifanikiwa kufuga nguruwe wengi sana waliompatia
kipato cha kutosha kuweza kuanzisha kampuni yake ya usambazaji wa nyama za
nguruwe alumaarufu kama kitimoto,na akapata mafanikio makubwa sana kupitia kazi
ile aliyokuwa anaifanya,
Funzo!
Hapa duniani ,vyeti vya darasani ni makaratasi
tu,cha muhimu zaidi je kichwani unayo akili ya maisha?
Kuwa na elimu ni muhimu sana ,lakini kuwa na
akili ya kutumia kipaji chako zaidi ni muhimu zaidi!
Kuna mtu mmoja alisema
Kipaji kinalipa kuliko hata taaluma
utakayoisomea.Ninakubaliana na huyu bwana kwa asilimia zote
FAIDA
ZA KUTUMIA KIPAJI CHAKO
Zifuatazo ni faida chache za kuamua kukitumia
kipaji chako au fani yako;
1.
UTAFURAHIA KAZI UNAYOIFANYA
Hapa Duniani
,hakuna kitu kizuri kama vile kufanya kazi au kitu unachokipenda.Bila shaka mtu
akiwa na kipaji maana yake ni kile kitu ambacho yeye mwenyewe
anakipenda,kwahiyo kwa mtu huyo kufanya kazi ile haitakuwa mzigo tena kwake.
Mfano mwingine ni huu!
Hakuna raha hapa Duniani kama kuoa au kuolewa
na mtu unayempenda kutoka moyoni
Ni furaha ya ajabu sana,na hata migogoro ndani
ya nyumba isiyokuwa ya msingi huwa inapungua
Sasa wewe oa au olewa na mtu usiyempenda,hata
akitokea nyumbani kwako utahisi kama mnyama Fulani ndiyo anaingia ndani ya
nyumba.
Nakushauri anza kufanya kitu cha kipaji
chako,hautaona shida kufanya ile kazi ,na hata kama utapitia changamoto katika
hiyo kazi ,itakuwa rahisi sana kwako kuweza kuivumilia na kupanda viwango
vingine katika kile unachokifanya.
2.
KIPAJI KITAKUPATIA UMAARUFU KULIKO KAZI ULIYO
ISOMEA
Hii ndiyo pointi ambayo hata mimi huwa
naifurahia sana .Maana hakuna mtu ambaye hapendi kuwa maarufu,
Sasa hebu jaribu kufwatilia katika watu maarufu
na wakubwa hapa duniani je kuna Profesa maarufu kuliko mwanamuziki maarufu?
Utagundua kuwa
Wasomi maarufu ni wachache sana,lakini watu
wanaofanya shughuli za vipaji huwa wanakuwa maarufu zaidi
Namaanisha kuwa ,watu wanaofanya shughuli za
vipaji huwa wanakuwa na mafanikio makubwa pengine kuliko hata wale waliosoma
sana
Naomba tuelewane vizuri hapa,simaanishi kuwa
watu wasisome ,hapana ,,ninamaanisha kuwa ukisoma ni vizuri,lakini ukisoma na
kukitumia kipaji chako ni vizuri zaidi.
3.
KIPAJI KINAKUPELEKA KUWA KARIBU NA WAKUU
Ni rahisi sana kwa muheshimiwa Rais wa Nchi
kukutana na watu maarufu wenye vipaji,kuliko kukutana na wasomi
Unaweza kuwa wewe darasa la saba tu ,lakini
unakipaji cha muziki,ukajikuta wewe unatumiwa sana na serikali yako katika
kugusa jamii katika maeneo Fulani Fulani,lakini mtu aliye na elimu yake
utamkuta yuko bize sana ofisini kwake
Unakuta mtu ni daktari,sasa muda wa kuwa karibu
na wakuu wa nchi atautoa wapi wakati huo kazi aliyoisomea itamtaka aende kukaa
hospitalini kutibu wagonjwa?
Ukitaka kuishi maisha ya uhuru na amani ,tumia
kipaji chako.
SHOW ME YOUR TALENT AND IWILL
SHOW YOU GREATNESS!
NASAHA ZANGU KWAKO!
Ukimuuliza
rafiki yako wa karibu kuwa yeye anamiliki nini katika maisha yake usishangae
kuona anakuorodheshea vitu vingi sana ambavyo yawezekana hujawahi kuhisi kuwa
yuko navyo,lakini cha kushangaza sana unaweza kuona amesahau kutaja fani
aliyonayo ambayo yamkini ndiyo inayompatia pesa za kuweza kukaa mjini.
Watu
wengi tumekuwa tukiishi maisha ya nje ya tulivyonavyo kwa muda mrefu kiasi
ambacho tunatumia muda mchache sana kufanya vitu ambavyo ni vya kwetu ila
asilimia 90% tunafanya vitu vya watu wengine.
Unapokuwa
unafanya kitu ambacho sio cha kwako kuna mambo mengi yanaweza kukukuta
MAMBO YANAYOWEZA KUKUKUTA
UKIWA UNAFANYA KITU KISICHOKUWA CHA KWAKO.
·
KUFANYA CHINI YA UBORA-yaani hata ukijitahidi
kiasi gani unaweza kujikuta bado haufikii ule ubora ambao hasa unatakiwa kwa
mtu wa kitu kile aufikie.
Nilipokuwa
bado mdogo nasoma shule ya sekondari ,nilikuwa napenda sana kufuatilia
michezo hasa mpira wa miguu,kwa bahati
mbaya sana mimi sikuwa na kipaji cha kucheza mpira.
Siku
moja kulikuwa na mashindano ya kimadarasa,kutokana na kuisha kwa wachezaji
katika darasa letu timu ya darasa letu ililazimika kuniingiza niweze kuwa moja
ya wachezaji uwanjani yaani first eleven.
Nilifanikiwa
kuingia uwanjani,lakini vituko vilivyoendelea uwanjani namwachia bwana.
Unajua
kitu gani kilitokea? Yaani ilikuwa kila nikipewa pasi moja ,kabla sijaipeleka
kwa mwingine ni lazima nianguke chini kwanza ,ile nasimama tu maadui
wameshakwapua mpira na kumpasia adui yangu nabaki nazunguka tu.
Basi
mdogo wangu alinikumbusha hadithi hii nikiwa nimekuwa mkubwa tayari nilicheka
sana maana nimegundua sasa kuwa kilichokuwa kinanitesa pale haikuwa kutokujua
mpira ,ila ilikuwa ni kufanya kitu ambacho hakikuwa fani yangu.
Sasa
nirudi kwako
Yawezekana
umehangaika kufanya kitu Fulani kwa muda mrefu sana,lakini kila siku umejikuta
unafanya chini ya ubora,wala usijilaumu ila shukuru Mungu kuwa leo hii umepata
majibu yako kuwa ni kwa sababu unafanya kitu ambacho siyo fani yako.
Asikudanganye
mtu!
Unapofanya
kitu ambacho ndichoulichoumbiwa kukifanya ,ubora wake utakaochipuka ni lazima
utakutambulisha tu kuwa wewe ni mtu wa namna gani.
Kwahiyo
hatupati shida kukutambua,maana ubora unaouonesha kwa kile unachokifanya
utatuambia kuwa je ni cha kwako au unaiga kutoka kwa watu wengine.
·
NGUVU KUBWA MATOKEO KIDOGO
Narudi
nyuma tena nikiwa shule,kuna jamaa alikuwa anapenda sana somo la hesabu lakini
kwa bahati mbaya sana kila akijitahidi alikuwa anafeli ,lakini mtu huyohuyo
alikuwa yuko vizuri sana katika masomo ya sanaa,kwahiyo pamoja na kuhangaika
sana katika somo la hisabati,ukimleta kwenye sanaa utaipatapata!
Pamoja
na juhudi zake zote za kulala darasani kusoma hesabu,lakini bado mtihani
alipata alama ya kawaida sana ambayo hailingani na juhudi alizokuwa amezitumia
katika kujiandaa.
Nataka
nikwambie!
Unatumia
juhudi kubwa lakini matokeo kidogo kwa sababu nyingi,ila kubwa huwa ni ile ya
kufanya kitu kisichokuwa fani yako.
Mimi
ni mwana muziki,najijua kuwa nimewekeza muda wangu mwingi sana katika kujifunza
kinanda kuliko gitaa,japokuwa gitaa pia naweza kulicheza bila shida,lakini
ukinipatia kinanda nitafanya kwa ubora zaidi kuliko gitaa,gitaa nitapiga tu
kawaida ambavyo mtu yeyote mwenye uelewa wa gitaa atasema na wewe ni miongoni
mwa wapigaji wa gitaa.
Lakini
nikicheza piano,mtu atakwambia we jamaa uko vizuri!
Natolea mfano jamani,maana tutaanza kugombana
na walokole wenzangu hapa mara oooh jamaa anajiinua na nini!
Tafadhali
sana ,huu ni mfano utakaoweza kukusaidia kuelewa ninachokifundisha.
Ukirudi
katika Biblia utakutana na jamaa mmoja anaitwa Daudi.Yule dogo aliitwa wakati
ambao Taifa la Israeli liko katika misukosuko mikubwa ya kivita,alitokea
mfilisti mmoja jina lake Goliath tena ambaye hajatahiriwa.
Daudi
alitakiwa kupambana na huyu Goliath,kinachonishangaza hadi leo ni kwamba,mfalme
alipojaribu kumpatia Daudi yale mavazi ya kivita na kombati za kijeshi,Dogo
aliamua kuzivua akasema hizi hazitanifaa,na wala hakutaka hata kuchukua siraha
za kisasa za kuweza kupambana na Yule mfilisti,
Unajua
ni kwanini?
Daudi
tayari alikuwa katika ARENA YAKE au
UWANJA WAKE WA KUJIDAI
Kwa
sababu hiyo Biblia inaeleza kuwa alichagua mawe laini matano,akatumia kombeo
kuweza kumpiga Yule Goliath,na kwa hakika Goliath aliuwawa na Daudi kiurahisi
sana,
Kile
ulichonacho kinauwezo wa kukufanya usitumie nguvu kubwa katika kupambana lakini
matokeo yakawa makubwa sana kwako.
1samweli 17;38-39,49-50
Daudi
akamuua Yule mfilisti kwa kombeo lake na jiwe laini.
Elewa kuwa ili ushinde au
upate matokeo makubwa ,sio lazima uwe na mtaji mkubwa lakini,ni lazima uwe
unafanya kitu kilicho sahihi kwako[yaani cha kwako].
·
KUKATA TAMAA MAPEMA
Moja ya dalili kuwa kitu
unachokifanya sio cha kwako ni ile hali ya kukata tama mapema
Nakwambia ukweli,kama kitu
kiko damuni yaani ni cha kwako,hauwezi kukikatia tamaa hata kama kimekukatisha
tamaa kiasi gani,
Mfano mzuri ni kwa mashabiki
wa mpira mfano SIMBA NA YANGA za Tanzania ambazo ni timu pinzani.
Kuna wakati timu yako
unayoipenda sana inafungwa zaidi ya mara mbili mfululizo ,lakini bado unakuta
mtu akikaa na washabiki wengine anajitangaza kuwa yeye bado ni shabiki wa timu
ileile iliyofungwa mara kadhaa,
Nataka nikwambie,kitu kama ni
cha kwako,haijalishi changamoto gani unapitia
bado kile kitu kitabaki moyoni mwako na ni lazima ipo siku utakifanya
tena.
Mfano.
Ikatokea umempenda mwanamke
Fulani au mwanaume Fulani ,hata itokee changamoto mbaya kiasi gani
ikawakosanisha ila lazima utajikuta mwisho wa siku moyoni unatamani kama vile
mngekuwa pamoja tena.ni kweli unaweza kuwa na ujasiri wa kusema muachane moja
kwa moja,lakini nakuhakikishia gharama
ya kumtoa mtu Yule moyoni huwa ni kubwa kuliko ngharama ya kuanzisha mahusiano
mapya.
Kwa hakika kitu kilicho cha
kwako ,hakiwezi kukufanya ukakikatia tama mapema,hivyo ukiona unakata tama
mapema maana yake ni kwamba hicho kitu sio cha kwako!.
Sasa basi ,hakikisha
unatambua kitu cha kwako ,ili ukianza kukifanya ukifurahie na uweze kupata
matokeo makubwa.Uzuri ni kwamba ,kitu kikiwa kwenye damu ,hata kama
hakitakulipa kwa wakati bado utakuwa na moyo wa furaha wa kuendelea kukifanya,
Kinachotakiwa sana hapa ni
ile furaha wakati unapofanya kitu chako,hakuna maana ya kufanya kitu ambacho
haukifurahii,unajiongezea stress katika maisha yako,
DHANA YA PLACEBO
KATIKA ULICHOKITEGEMEA
Kwa namna moja au nyingine,unaweza
kujikuta wewe unapendelea kitu Fulani,lakini kwa namna isiyokuwa ya kawaida
ukajikuta umepata kitu kingine tofauti na kile ulichokipenda ,lakini
kikakupatia uwezo wa kupata fedha nyingi na wakati mwingine ukaona kama
kinaziba lile pengo la kukosa kile ulichokitegemea kwa muda mrefu.
Katika lugha ya kitaalamu
tunaita PLACEBO ACHIEVEMENTS au
Mafanikio mbadala
Placebo-ni kile kitu kinachofanania na ukweli
lakini sio kweli
Mfano
Mtu anayeamini sana nguvu ya
dawa,kila anapoumwa ,siku anakuja kwako daktari ukaona huyu hana shida lakini
ili awe sawa kisaikolojia ni lazima apewe dawa za aina Fulani hata kama
hazitibu kile anachoumwa ila zitamfanya aamini kuwa amepewa dawa sahihi na
atapona.
Wakati huo ukimpatia hata
panadol tu ,jamaa ananyanyuka kitandani na kuamini kuwa ametibiwa vizuri na
amepona
Sasa hata katika maisha yetu
,kuna wakati Mungu huwa anaruhusu placebo zitumike katika maisha yetu ili
kututia moyo mahali ambapo anaona kabisa tumeinama sana mioyo yetu.
Unakumbuka kilichotokea kwa
Ibrahimu alipokuwa hapati mtoto kwa muda mrefu,jamaa hata ngazi ya uvumilivu
ilianza kupotea ,ikabidi Mungu atumie placebo ya ISHMAILI ambaye kimsingi sio mtoto
wa mkewe Sarai .
ISHMAILI anazaliwa kwa
kijakazi wa Sarai ,anakuwa faraja kidogo kwa Ibrahimu na Sarai ,lakini bado Mungu
anasema Atampatia Ibrahimu mtoto atakayekuwa mrithi kupitia tumbo la Sarai
mkewe.Hapa tunaona uwepo wa ISHMAILI ni Placebo tu,lakini ISAKA MWENYEWE anakuja kuzaliwa baadaye
Mwanzo 16;15-16
KAZI YA PLACEBO
·
Kukutia moyo ukikosa ulichokitegemea
·
Kulinda heshima yako
·
Kukuongezea imani
Ushauri wanguJitahidi sana
usiridhike na placebo,tafuta kwa bidii kile kilicho halali yako!
SEHEMU YA TATU
WEWE NI
NANI?
Natumai katika sura iliyopita
nimejaribu kukufungua macho yako ili uweze kutambua mlengo mkuu wa kitabu hiki
na somo hili la THE POWER OF YOUR
POSSESION
Kiujumla ninazungumzia uwezo
wa kitu ulichonacho au kipaji chako,ndoto yako ,namna ambavyo kinaweza kukusaidia
kufikia malengo yako na mipango yako katika maisha.
Kile unacho kifanya ,ndicho kinachokutambulisha
Hutatakiwa kutumia matangazo
ya hadhara kujitambulisha kuwa wewe ni muimbaji ,lakini kazi unayoifanya ndiyo
itakayokutambulisha.
Nilipoanza kwa mara ya kwanza
kuandika sermon zangu za OGS[online Gospel Sermons] wala hata sikuanza kujitambulisha
kuwa mimi ni mwalimu, lakini kadiri siku zilivozidi kwenda nikakuta watu
wananijia inbox na kuniita mwalimu wa neno la Mungu,na wengine wakaenda mbali
sana wakaanza kuniita Mtumishi na wengine wakaniita Mchungaji.
Nataka niseme hivi!
Siyo lazima ujitambulishe
kuwa wewe ni nani,ili watu waanze kuja kwako kupata aina ya huduma unayoitoa
,ila huduma unayoitoa au unayoifanya ndiyo itakayo kutambulisha kwa watu, na
wao ndio watakao kutafuta.
Nakumbuka kipindi cha mitume
katika kitabu cha matendo ya mitume,watu walipoona Petro anafanya mambo makubwa
,na kuna wakati hata kivuli chake tu kinaponya wagonjwa wao,ndipo watu wakazidi
kumsonga Petro na watu wengi wakamwendea kupata huduma ,na ghafla umaarufu wa Petro
ukaenea sana kwa zile kazi alizokuwa anazifanya za kuihubiri injili ya YESU KRISTO.
KAZI
unazozifanya ndizo ambazo zitakutambulisha mbele ya mataifa na wanadunia wote,
Kuna mtu anasema;
Ningekuwa maarufu ningeanzisha
biashara ya kuuza juisi ya embe!
Sasa kanuni iko hivi
Anza kuuza juisi ya embe ukiwa bado haujajulikana
,halafu kupitia kazi hiyo unayoifanya utatambulishwa kuwa wewe ni muuzaji bora
wa juisi ya embe halafu utakuwa maarufu na wateja wako watakuwa ni wengi
kupindukia.
Kuna watu wengi sana
,wanasingizia kutokufahamika kwao kama sababu ya kutofanya mambo Fulani katika
maisha yao,lakini ukweli ni kwamba KAZI
UNAYOIFANYA NDIYO ITAKAYO KUTAMBULISHA WEWE NA KUKUPATIA UMAARUFU UNAO UTAKA.
Ndugu yangu ,hii ni kanuni ya
Kimungu na hakuna anayeweza kuipindua,unafanya kazi. ,kazi inakutambulisha
katikati ya mataifa.sasa ni uamuzi wa kwako wewe kuamua aina gani ya kazi
unayotaka ikutambulishe.
Mifano ya watu
waliotambulishwa kwa kazi zao katika Biblia
1.PETRO.
Matendo 5;16-17
Huyu jamaa kwa kufanya kazi
ya Mungu kwa uaminifu ,umaarufu wake ulichipuka na kuenea kwa haraka sana ,watu
wakawa hata wanawaleta wagonjwa wao ili tu kivuli cha Petro kiwapitie wakawa wanapona.
2.YUSUFU
Mwanzo 37;5
,37;9 mwanzo 41;25
Jamaa kupitia kazi yake ya
kutafsiri ndoto za watu anapata umaarufu na kuwa Waziri mkuu wa Nchi ya Misri.
3.MUSA&HARUNI
Kutoka 7;19,
Kutoka 8;5, Kutoka 10;12-14
Kupitia kazi ya kuwaombea tu
Ruhusa wana wa Israeli watoke Misri ,Musa anakuwa maarufu sana kwa Farao
Hivi ungekuwa ni wewe
ungejisikiaje yaani unafanya kazi ambayo inakusogeza karibu na mkuu wa nchi
kiasi ambacho mnajadiliana kwa pamoja?
Ingekuwa
ndiyo Dunia ya sasa au Tanzania ya sasa kesho yake ungeshangaa katika vyombo vya
habari wanaandika!
Breaking news -MUSA AONGEA NA
RAISI NA KUMWAMBIA ATALETA VYURA TANZANIA NZIAMA !
Nakwambia ukweli,ingekuwa ni
sasa ukifanya kazi kama aliyoifanya musa utajikuta dakika chache, umejulikana
Dunia Nzima.
Nataka nikwambie kitu
Wewe ukitaka kutambulishwa ,basi chagua kazi
maalumu utakayoanza kuifanya ,hata kama ni kuuza maandazi ,ukifanya kwa
uaminifu utashangaa mji mzima wanakutambua kama Muuzaji maarufu wa maandazi
bora ,na unapotambulika ndiyo sasa unapata wateja wengi na umaarufu wako unakua.
Sasa nina ugomvi mdogo na wakristo ambao
hawaamini katika umaarufu.utanisamehe sana katika hili,Ila ukweli nikwamba
,unapoanza kufanya jambo kwa uaminifu Mungu huwa anakutambulisha kupitia kazi
unayoifanya ,na baada ya hapo umaarufu unakuwa ni sehemu ya maisha yako hasa
pale unapofanya kitu cha ndoto yako.
NAMNA YA KUCHAGUA KAZI ITAKAYO KUTAMBULISHA
Sasa katika mfumo wa maisha yako ,naomba
nikufundishe njia ya kuchagua aina ya kazi ambayo ungetaka ikutambulishe.na kwa
hakika kama utatumia vigezo hivi ,aina hiyo ya kazi itakufanya ufanikiwe haraka
na uwe vile ulivokuwa unaota maisha yako yawe siku zote;
Tumia vigezo vifuatavyo;
·
Kazi unayoichagua iwe ni kazi ambayo unaipenda
kuliko kazi zote,.
Yaani kwa mfano mtu akaja kwako akiwa na pesa
Bilioni moja halafu akakuuliza ungependa ufanye kazi gani endapo nikikupatia
hizi pesa,kile kitu cha kwanza utakachokichagua kutoka moyoni ndicho hicho kiko
katika damu yako na ndiyo kusudi la kuumbwa kwako
·
Iwe ni kazi ambayo msingi wake haujengwi kwa
mtaji wa pesa.
Pesa huwa ni matokeo tu ,wala haipo katika
mlinganyo wa kuanza kitu Fulani[equation]Namaanisha
kuwa ,kitu ulichozaliwa nacho,hakitegemei uwepo wa pesa ndipo kiweze
kutekelezeka ,ila kinategemea maamuzi ya mfanyaji kwa maana tunatambua kipaji
cha mtu kwa urahisi sana pale ambapo anakuwa hana pesa.
Mara nyingi mtu akiwa hana pesa ,kuna aina
Fulani ya vitu anapendelea kuvifanya ,na wakati mwingine huwa wakati wa
mapumziko akitoka kazini anakohangaikia tumbo lake, akirudi nyumbani anaanza
kufanya kitu anachokipenda kuliko vingine vyote.
Zamani wakati tunakua,tulikuwa tukitoka shule
tunachukua mwiko wa kusongea ugali na kuanza kuigiza kama vile tunapiga gitaa
wakati huo tukiimba sauti za gitaa midomoni mwetu ,mimi pamoja na kaka yangu,ilifika
wakati hadi mama akawa anatuchapa kwa sababu saa zingine tunachukua mwiko
masafi halafu tunaanza kuuchezea mithili ya wanaopiga magitaa.hii hali badaye
iliendelea ikatuletea hali ya kugundua kuwa kumbe sisi ni wanamuziki kwa asili
yetu ya ndani ,na ndiyo maana tulipoanza kujifunza masomo ya muziki haikuwa
kazi ngumu kabisa kwetu,kuna wakati tulikuwa tunauelewa wa muziki kabla hata mwalimu hajatufundisha.
Sasa ni mara ngapi umeona mtoto wako anafanya
vitu ambavyo vinafanania na kitu Fulani halafu ukakipuuza? Mfano unaona mtoto
wako anatengeneza magari ya vikopo wewe unamkemea na kumchapa.ingekuwa ni baada
ya kujifunza somo hili ungetakiwa sasa kuanza kumlea huyo mtoto katika misingi
ya uhandisi wa magari,na yamkini hata aina za shule ambazo utampeleka
zinatakiwa kuwa ni shule za ufundi .ufurahi maana tayari una muhandisi wa magari katika nyumba yako.
Baada ya kukueleza mambo hayo sasa,chukua muda
kutafakari ni kitu gani ambacho unao uwezo wa kukifanya kwa ubora kabisa? Hicho kitu kwa hakika ndicho
ambacho kitakutambulisha kuwa wewe ni nani.
SEHEMU
YA NNE
UNANINI
MKONONI MWAKO ? [MTAJI]
Katika
sehemu iliyopita nilikuwa nikizungumzia
kwa habari ya namna ya kujua wewe ni nani?
Tumeona
mambo ya msingi unayotakiwa kuyafanya kabla ya kuamua kuanza kufanya jambo
Fulani katika maisha yako ,ambalo unategemea likuletee mafanikio makubwa katika
maisha yako.Nimeeleza kuwa ,hata kama jambo unaliona kuwa ni dogo sana lakini
unao uwezo wa kulitumia hilohilo likaleta matokeo makubwa sana katika maisha
yako .
Katika
sehemu hii ya nne, nataka tujiulize swali hili je UNANINI MKONONI MWAKO?
Maana
ya swali hili kwa lugha nyingine ni je KITU GANI KILICHOKO NDANI YA UWEZO WAKO?
Ndugu ya mpendwa
Kati
ya swali la muhimu sana katika maisha yako ni kujiuliza na kujua kitu gani
ambacho uko nacho mkononi ambacho kinaweza kutumika kama kianzio katika kupata
vitu bora ambavyo Mungu amekuahidia.
THE POWER OF YOUR POSSESION imelenga kukutambulisha uwezo au matokeo
makubwa ambayo kitu kidogo ulichonacho kinaweza kukuletea katika maisha yako.
Je
,hicho kitu kidogo ni kipi?
Ni
ufundi ulionao[fundi seremala?
Fundi
redio?
Fundi
uashi?
Mwana
muziki chipukizi?
Mfanya
biashara?
Ni
mtumishi wa uma?
Hivi
vyote ni moja tu kati ya maswali unayotakiwa kujiuliza kuwa uko na kitu gani?
Na inawezekana ikawa zaidi ya hayo wewe ni mwalimu,muhandisi,daktari,mkulima
,mfugaji,producer wa muziki ,mpiga picha,muhubiri,mama lishe nk;
Hivi
vyote ni vitu unavyoweza kuwa navyo
Shida
sio kuwa na hivi vitu,ila shida je unamaelekezo sahihi ya namna ya kuvitumia
ili vikuletee matokeo makubwa unayoyataka katika maisha yako
Yaani
unajua namna ya kuvitumia ili uione nguvu iliyomo katika hivyo vitu?
Sasa
tuanzie hapa.
Kila
kitu ulichonacho kinakuwa na thamani kwako pale ambapo unakuwa na maelekezo sahihi
ya kukitumia na hatimaye kinakupatia matokeo makubwa /kinakufaa sana.
Mfano
Wewe
unaweza kuwa na simu [smartphone]lakini usijue namna ya kuitumia ,kwahiyo
utaishia kupiga na kupokea ,pamoja na kutuma na kupokea sms tu! Usijue kuwa
kuna watu kupitia simu hizohizo wameweza kutengeneza na kupromote biashara zao
na kujitangaza kibiashara na wanapata pesa nyingi kupitia simu.
Hapa
ndipo utakapogundua kuwa ,shida sio kuwa na fani Fulani au kitu Fulani au kazi
Fulani,ila shida iko hapa je unayo maelekezo sahihi ya namna ya kukitumia hicho
ulicho nacho?
KUTOKA KATIKA BIBLIA
Naomba
sasa nikupitishe katika Neno la Mungu kukuonesha jinsi ambavyo watu walikuwa na
vitu kama walivyonavyo wengine ,lakini baada ya kupewa maelekezo ya namna ya
kuvitumia viliweza kuleta mabadiliko na matokeo ya ajabu sana .
1.MUSA & FIMBO YAKE;
Kutoka 7;19
Bwana akamwambia Musa,mwambie Haruni ,shika
fimbo yako,kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri,juu ya mito yao,juu ya
vijito vyao,na juu ya maziwa ya maji yao,na juu ya visima vyote vya maji ili
yageuke kuwa Damu ,nako kutakuwa na Damu katika nchi yote ya misri katika vyombo vya mti na katika vyombo vya
jiwe.
Katika
andiko hili utaona mstari ule wa 20 pale chini .Baada ya Musa kufanya kama
walivyopewa maelekezo ,maji yote ya misri yakawa damu!
Kutoka 8;5
Akapewa
tena maelekezo ya kuitumia fimbo yake ,ikaleta vyura katika nchi ya misri
Kutoka9;22
Akapewa
tena maelekezo ya kutumia fimbo yake ,kukaja mvua kubwa ya mawe katika Nchi ya
misri.
Unaweza
kuona jinsi gani FIMBO kitu kidogo kabisa alichokuwa nacho Musa kilivoweza
kuleta matokeo makubwa sana baada ya kuwa kimetumika sawasawa na maelekezo
maalumu.
Nataka nikwambie!.Kupitia ujumbe huu wa THE POWER OF YOUR POSSESION Mungu
amenipatia neema ya kukueleza namna ambavyo utatakiwa kuvitumia vitu
ulivyonavyo hata kama ni vidogo kiasi gani ili kusudi kupitia hivyo viweze
kuleta matokeo makubwa katika maisha yako.
2.CHUPA
YA MAFUTA & MWANAMKE MJANE
2falme 4;2
Elisha akamwambia ,nikufanyie
nini?
Niambie una kitu gani
nymbani?,akasema mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani ,ila chupa ya mafuta.
Kupitia mfano huu,huyu mama hakuona kama chupa
yake ya mafuta ilikuwa na msaada kwake tena baada ya kuwa mume wake amekufa ,na
amemwachia madeni,lakini habari njema ni kwamba ,kupitia kile alichokuwa nacho yaani
chupa ya mafuta ,alipopata maelekezo kutoka kwa ELISHA ,alikuwa tajiri wa
mafuta.
Ukiendelea pale mstari wa 3……. Utaona mchakato
mzima jinsi ulivyokuwa.
Masikini mama wa watu .ana madeni ,lakini
anapokwenda kwa yule mtumishi wa Mungu akidhani labda anaweza kupata msaada wa
pesa au vitu vikubwa vitakavyomsaidia kulipa madeni ,anakutana na swali gumu
sana linalomtaka yeye mwenyewe aanze kujitathimini kuwa ana nini mkononi mwake,
Kuna wakati mwingine huwa tunamwendea Mungu
tukiwa tunahuzuni sana tukidhani kuna vitu vikubwa sana ambavyo Mungu anaweza
kuvitumia kubadilisha maisha yetu,lakini ukweli nikwamba ,chochote kile
ulichonacho utakapopata maelekezo sahihi ya namna ya kuanza kukitumia kinauwezo
wa kubadilisha kabisa maisha yako,
1falme 17;12
Bado biblia inaeleza kwa habari ya mjane
mwingine aliyekuwa hana chakula na wakati huo ulikuwa ni msimu wa njaa,kupitia
maelekezo aliyopewa na mtumishi wa Mungu alipata neema ya chakula cha kumtosha
kuvuka msimu wote aliokuwa anaupitia katika maisha yake.
Shida sio kazi gani unayoifanya,shida ni je una
maelekezo sahihi ya namna ya kuifanya hiyo kazi ikuletee matokeo makubwa?,lakini
sharti ni kwamba hiyo kazi iwe ni ya kwako.ndio maana swali la kwanza kwa wale
akina mama pamoja na musa pia ni UNANINI MKONONI MWAKO?
YAANI ,KITU GANI AMBACHO NI
CHA KWAKO TUNAWEZA KUKITUMIA KUFANYA MAAJABU?
3.KIPAJI NA YUSUFU
Mimi huwa nasema ,kati ya watu ambao walikula
bata kiulaini katika maisha yao ,ni pamoja na yusufu.alipata umaarufu kwa kitu
kidogo sana .yaani kile kipaji tu cha kutafsiri ndoto ,hatimaye kinamfanya
anakuwa WAZIRI MKUU.Hii inanipa moyo sana kuwa kitu chochote maadamu tu ni cha
kwangu,endapo nitakitumia vizuri kwa msaada wa Mungu naweza kufanya mambo makuu
Mwanzo 41;25, Vilevile Katika Ebrania
13;6 biblia inasema Bwana ndiye
anisaidiaye ,sitaogopa!
SEHEMU
YA TANO
NAMNA YA KUANZA KUKITUMIA ULICHONACHO
Kila kitu huwa kina kanuni zake,
Katika sura hii nategemea sasa tayari umekwisha
jitambua kuwa wewe ni nani ,na umeumbwa kwa kusudi gani,na kitu gani unatamani
kuanza kukifanya .kama endapo umegundua kuwa yamkini ulikuwa unafanya kitu
ambacho siyo cha kwako ,au ulikuwa unafanya kitu ambacho ni placebo,lakini sasa
unataka kuanza kufanya kitu sahihi kwako.Maelekezo yafuatayo yatakusaidia sana
kama ukizingatia kwa umakini na kuyafuata.
Unapotaka kuanza kufanya kitu cha ndoto yako
,fanya mambo haya ;
1.TENGENEZA
SHAUKU YA NDANI IFIKE KIWANGO CHA KUTOVUMILIKA
Kwa lugha nyingine[Create your ambition to the
level of intollelance]
Moja kati ya sermon nilizoziandika tarehe 16,17
januari ilikuwa inasema LET YOUR ANGER
MOTIVATE YOU!
Unapofikia pointi ya kukionea hasira kitu
kinachokutesa ,unapata nafasi ya kutengeneza mazingira mazuri kwaajili ya kuchomoka
katika eneo ulilopo.
Mfano
Ikiwa wewe umechoka na maisha ya kupungukiwa
pesa ,au umasikini kwa ujumla wake,ile hasira ya ndani inapozidi uvumilivu wako
utatafuta njia yeyote ile ili uweze kuepukana na umasikini .Sasa usinielewe
vibaya ,maana ya umasikini sio kukosa pesa tu kama wewe unavyotafsiri.Wakati
mwigine umasikini huwa ni kutoweza kufanya jambo ambalo ni sehemu ya maisha
yako au kutoweza kutimiliza malengo ya maisha yako.
Kwa maana hiyo,umasikini ni hali yeyote ile
inayoweza kukuzuia wewe kutimiza ndoto yako.unaweza kuwa na pesa za kutosha
sana hata za kuwapatia wengine ,lakini kama umeshindwa kutimiza ndoto yako basi
wewe ni masikini wa uwezo wa kutimiza ndoto zako.
Sasa hatua ya kwanza ili uweze kutimiza ndoto
yako ni kutengeneza shauku ya ndani itakayokuwa na nguvu ya kupenya kila aina
ya changamoto mradi tu ufikie ndoto yako.
AZIMIA KUTOKA MOYONI!
2falme 7;3-5
Hapa biblia inawataja wakoma wanne ambao ilifika
wakati wakaona hawana njia nyingine zaidi ya kuamua kwenda upande wa adui zao
yaani LIWALO NA LIWE!
Walipoamua kuanza kwenda ,ndipo hapo Bwana
akasikizisha kishindo cha miguu yao mbele ya adui zao na hatimaye adui
wakawakimbia wakoma.
DECIDE TO START! .DECIDE TO
MOVE! ,DECIDE TO DO!
2falme 5;1-14
Hapa tunakutana na Jemedari wa vita NAAMANI
lakini huyu jamaa alikuwa na ukoma.akaamua kutoka moyoni kuwa anataka kupona
Yale maamuzi ya ndani ,yalimfanya pamoja na
ujemedari wake wote ,aende akajirushe katika mto yoldani mara saba
Kumbuka kwa nafasi yake ya kiserikali kwenda
kuanza kujitumbukiza katika mto yolodani,mto mchafu,ilikuwa ni fedheha kubwa
sana kwake,na ndio maana ukifwatilia utagundua kuna wakati alitaka kukataa
kufuata maelekezo lakini watumishi wake wakamshauri ,alipoamua kwenda kuanza
kujichovya katika mto yolodani mara saba ndipo akatoka akiwa na ngozi nzuri
kama ya mtoto mchanga.yaani ukoma wake ukamachialia.
Nataka nikwambie
Maamuzi ya kuamua kutoka hapo ulipo na kuanza
kukitumia kile kipaji chako au kuanza kufanya kazi ambayo ndiyo ndoto yako
yanakutaka wewe mwenyewe usiwe mtu wa kuteteleka kimaamuzi.Ukiisha amua ,amua
kwenda mbele moja kwa moja ,hapo ndipo mwanzo wa mafanikio yako utafunguliwa
rasmi.
2.TAFUTA WATU SAHIHI
Katika kila kitu unachokifanya huwa kuna watu
ambao ni tayari wamebobea katika eneo hilo.kama ukitaka kuanza kufanya kile
kitu utatakiwa kupata taarifa sahihi kutoka kwa watu sahihi.ninaposema watu
sahihi ninamaanisha kuwa wale watu wenye ujuzi na maarifa sahihi kuhusu fani
yako
Mfano.
Kama wewe unataka kuwa mwanamuziki bora ,sharti
la kwanza hakikisha unakutana na wanamuziki ambao watakuambukiza maarifa sahihi
kuhusu muziki.
Utakuwa mtu wa ajabu sana kama wewe una fani ya
biashara,ila unaenda kuomba ushauri wa kibiashara kwa afisa mifugo au kwa mkulima.
Ninachojaribu kukueleza hapa ni ile hali ya
kuamua kutafuta mahali maarifa sahihi kuhusu kitu unachokifanya yanapatikana.
KUTOKA KATIKA BIBLIA
Kwakuwa neno la Mungu ndio muongozo wetu ,hebu
tutumie dakika hizi chache nikupitishe kwa watu kadha wa kadha ambao walitafuta
watu sahihi katika kufanya au kutimiza ndoto zao.
A.NAAMANI ALIMTAFUTA ELISHA
2falme 5;3
Naamani alipogundua kuwa ana tatizo la
ukoma,aliamua kwenda kwa mtu sahihi anayeweza kumsaidia katika tatizo au ndoto
yake ya kupona,ndio sasa akafunga safari kwenda kwa Elisha.
B.SAULI[PAULO] ALIMTAFUTA ANANIA.
Jamaa mwingine ambaye alikutana na mtu sahihi
ndoto zake zikaanzia pale kutimia ni Paulo aliyekuwa sauli kwa wakati ule,huyu
Bwana alikutana na Anania ndipo alipoombewa na kupata kuona tena.
Matendo 9;1-16,17-18
Ndoto yake ya kuona ,inawezekana isingetimia
tena ,ila mtu sahihi aliyeandaliwa kwaajili yake alipokutana nae na kumpatia
maelekezo pamoja na maombezi ndipo Sauli akapata kuona tena na ndiye Paulo
mtume.
Ninachojaribu kukueleza ni kwamba ,jitahidi
sana kutafuta watu sahihi ambao wamebeba vitu kama vya kwako .
3.CHAGUA MBINU YA KWAKO YA
KUITUMIA[CHOOSE YOUR STYLE]
Kati ya jambo ambalo linatukwamisha watu wengi
sana katika harakati za kuanza kuzitumia fani tulizonazo au kipaji au kutimiza
ndoto zetu ni ile tabia ya kuiga watu wengine na kutaka kukopi au kuiga kila kitu ambacho wanakifanya wengine katika
eneo hilo.Nimekutana na wahubiri wa injili wanaochipukia wamefikia hatua ya
kuiga hadi sauti za watumishi wakubwa ambao wamekuwa wakiwafwatili,binafsi
sipendi sana mtu anayependa kuigaiga na kukopi mambo ya watu wengine,japokuwa
Biblia inaeleza kuwa tuige yaliyo mema,ila haikumaanisha tukose mbinu za kwetu
za kiufunuo wa kwetu.ushauri wangu kwa waimbaji wa nyimbo pamoja na wahubiri,hebu
tafuta style ya kwako ambayo Mungu amekupatia kama njia ya kufikisha ujumbe kwa
watu wake.acha tabia ya kuiga iga huduma za watu.
Hasara za kuiga ni kwamba ,utatumia nguvu kubwa
sana kufanya kitu halafu wala usikifanye kwa ubora uliokuwa unatakiwa
Kwa bahati nzuri sana Mungu wetu ameandaa mbinu
ya kwako peke yako katika kila kitu ambacho amekupatia kukitekeleza.
Na hata katika biashara yako,ukiishia kuiga
wengine wanachokifanya unaendelea
kuwapatia soko wale unaowaiga ,ila hautangazi soko lako mwenyewe.
Sasa katika kuanza kutumia fani yako au kipaji
chako,au chochote ambacho ndicho ndoto yako hakikisha una mbinu ya kwako peke
yako utakayoitumia kutekeleza kile kitu
Nina uhakika Mungu wetu anazo njia nyingi sana
za kukusaidia kujua ni kwa namna gani uanze kutekeleza yale unayotakiwa
kuyatekeleza.
KUTOKA KATIKA BIBLIA
Hebu turudi kwenye katiba yetu mara moja
Yoshua 6;3-20
Ebrania 11;30
Hapa inaelezea jinsi ambavyo Yoshua alitakiwa
kuwaongoza wale wana wa Israeli katika kuuingia mji wa Yeriko,Kinachonishangaza
hapa ni ile mbinu ya kivita ambayo ilitumika wakati ule .
Ni kweli tumezoea kuona watu wanaoingia katika
vita na kuvamia mji ambao ni boma ni lazima waende pale wakiwa na siraha
mbalimbali zitakazowasaidia kupambana na hatimaye kuingia katika ule mji na
kuteka nyara.Lakini Biblia inaeleza kuwa ,Mungu alimpatia mbinu ya tofauti
kabisa mtumishi wa Mungu Yoshua,badala ya kwenda na siraha kubwa wao waliambiwa
waende na vitu kama;Matarumbeta,Kupiga
makelele na Kuzunguka ukuta mara saba.
Ninauhakika asilimia mia moja kuna baadhi ya
watu mle ndani walikuwa wanamcheka Yoshua kiongozi wao moyoni,kuwa jamaa sasa
anazeeka vibaya jamani.sasa anatuambia
tukapambane vita ili tuteke mji wa Yeriko na matarumbeta badala yakatumike kuimba kwaya huko!
Sijajua ungekuwa ni wewe mwenzangu uko miongoni
mwa wale jamaa ungesemaje pia ,yamkini ungekuwa na maneno mengi ya kumshauri
Yoshua kwa kuhisi amechanganyikiwa,lakini nikwambie tu kuwa;
Mungu anapokupatia kitu cha
kufanya ,huwa anakupatia na mbinu za kukitimiza hicho kitu.
Kwahiyo ni jukumu lako kuanza kutafuta mbinu ya kwako ya kuweza kuanzisha kitu cha kwako
Kuwa wa tofauti na wengine,ule utofauti ndio
ambao utakutambulisha wewe kama mtu wa pekee.
4.
KUWA KATIKA MAZINGIRA SAHIHI
Moja kati ya vitu ambavyo huwa vinatufanya
tushindwe kuanza kufanya vitu ambavyo ni ndoto zetu ni mazingira.Kuna mazingira
mengine kwakweli huwa yanakatisha tama sana,sasa kuna watu huwa wanajifanya wao
ni mabingwa wa kuvumilia ugumu wa mazingira,mwisho wa siku mambo yao
yanaharibika kwa sababu za kimazingira.
Nchi na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana ,na
tena Mungu wetu ametupatia kumiliki vitu vyotee na kila sehemu tutakayo
ikanyaga tumepewa na Bwana.
Sasa wewe kama hutaamua kutafuta mazingira
mengine yatakayokubeba katika kile kilichopo ndani yako ,usitegemee kuinuka na
fani yako,Japokuwa ni kweli Mungu anaweza kukuambia ukae eneo fulani hata kama
ni gumu sana kiuchumi,ila hakikisha ni yeye ndiye kasema ,na huwa anakusudi
maalumu kwa ajili yako
SHUKRANI
Ninamshukuru sana Mungu kwa neema na uzima ,na
kunipatia uwezo wa kuandika kitabu hiki.sifa na utukufu zimrudie yeye.
Ninamshukuru mkewangu kipenzi Irene Benny
Chavala,kwa kuwa mke bora na kunishauri katika mengi wakati nikiwa naandika
kitabu hiki,huduma yako ni kubwa mkewangu asante sana kwa kuwa mama mlezi bora
wa huduma yangu.
Ninawashukuru wanafamilia wote wa OGS na uongozi mzima wa GOSPEL SERMON MINISTRIES ambao wamekuwa bega kwa bega wakiniunga mkono na
kunishauri kazi nyingi tunazotakiwa kuzifanya katika huduma hii ikiwa ni pamoja
na MR
PHILIPO PH Mungu akubariki
sana.
Ninamshukuru sana Mchungaji wangu mlezi wa
kanisa la TAG Bethel Mahenge Pastor Charles Njobero Kwa kutambua
huduma iliyoko ndani yangu na kunishauri kuanza kuifanyia kazi kwa kuandika vitabu ,baba Mungu akubariki sana .
Mwisho kabisa nikushukuru wewe ambaye umeamua
kupata nakala ya kitabu hiki ,wewe ndiye unayetufanya tukeshe tukimtafuta Mungu
atupatie ufunuo mpya kwaajili ya kazi yake kwako.nasema MUNGU AKUBARIKI SANA.
KUHUSU MWANDISHI.
Ezekia Chavala,ni kijana Aliyeokoka na ameoa,yaani ni mume wa mke mmoja ambaye ni mwanamke,na pia ni Afisa Afya kwa taaluma.
Ezekia Chavala ni mwanamuziki wa muda
mrefu,mtaalamu wa kinanda na gitaa .Pia Ezekia chavala ni producer wa nyimbo za
injili,na mwalimu wa muziki ,anafanya kazi za kuwaandaa kwaya mbalimbali
wanaotaka kurekodi ,kuwafundisha nyimbo na kuwaingiza studio moja kwa moja.
Ezekia chavala ni mwalimu anayefundisha Muziki
mitandanoni,na kwa sasa yuko na KINGDOM
MUSIC SCHOOL ONLINE [KIMS] kwenye group la watsap!
Pia mr Chavala ni Mwalimu wa Neno la
Mungu,anafundisha watu Neno la Mungu katika makanisa mbalimbali na mitandaoni.
Mr Chavala pia ni Mwandishi wa vitabu,majarida na
makala mbalimbali za Neno la Mungu na maisha kwa ujumla wake.
Ezekia chavala pia ni muimbaji wa nyimbo za
injili,na ni mwalimu wa Kusifu na
kuabudu ,na mpigaji wa vyombo kanisani.
Binafsi najisikia FAHARI kumtumikia Mungu.
Ukitaka kujiunga na shule ya muziki online[KIMS]
–tuma ujumbe mfupi kwenda namba -0621029725
Kwa maswali na maoni tuandikie
simu;+255621029725
+255677904755
Karibu sana GOSPEL SERMON MINISTRIES[GSM]
KAZI NYINGINE TUNAZOZIFANYA;
Tunafundisha muziki online,tunatoa articles za
Neno la Mungu Online,Tunatoa ushauri wa kiafya,tunaandaa matamasha mbalimbali ,tunafundisha
kuhusu ujasiliamali!
Tunapatikana
MOROGORO-MAHENGE –TANZANIA.!
No comments